DAR ES SALAAM, Tanzania: Rais wa Uganda, Yoweri Museveni anatarajiwa kuwasili nchini kesho Jumamosi, Februari 7, 2026, kwa ziara ya kikazi ya siku moja.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Februari 6, 2026 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, imesema Rais Museveni atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan, yakilenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa miongoni mwa ajenda kuu za mazungumzo hayo ni masuala ya nishati, hususan Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), unaotarajiwa kuleta manufaa kwa Tanzania, Uganda na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.
Viongozi hao wawili pia wanatarajiwa kujadili masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa yanayogusa maslahi ya pande zote mbili, ikiwemo biashara, usalama na miundombinu.









