DODOMA, Tanzania: WAZIRI Mkuu Dk Mwigulu Nchemba, ameipongeza timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Tanzania (Taifa Stars) kwa kufikia hatua ya 16 bora fainali za Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2025 zilizomalizika mwezi uliopita nchini Morocco na kwamba mafanikio hayo yameitambulisha zaidi Tanzania.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba, Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Februari 6, 2026 kwenye hotuba yake ya kuahirisha shughuli za Bunge la 13 Mkutano wa Pili ulioanza Januari 27, 2026.
“Nitumie fursa hii adhimu kuipongeza Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu (Taifa Stars) kwa kufanikiwa kuandika historia kwa kufuzu hatua ya 16 Bora ya Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
“Tangu kuanzishwa mashindano haya, Tanzania imefanikiwa kushiriki mara nne, mwaka 1980 nchini Nigeria; mwaka 2019 nchini Misri; mwaka 2023 nchini Ivory Coast na mwaka 2025 nchini Morocco ambapo tumeweka rekodi ya kuingia 16 bora.
“Mashindano ya AFCON hutazamwa na watu wengi duniani, hivyo, mafanikio haya yameiwezesha Tanzania kutambulika zaidi katika ramani ya soka barani Afrika na duniani kote,” amesema Dk Nchemba.








